7 Aprili 2025 - 22:57
Source: Parstoday
Ulaya inapoteza itibari ya kimaadili kwa kuitetea Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Iran amesema bara Ulaya linapoteza itibari ya kimaadili kwa kuutetea utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa msingi huo itajipata katika upande mbaya wa historia.

  Ismail Baghaei Hamaneh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Iran, kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii X, siku ya Jumapili aliandika kuwa:

“Uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati ya kukamatwa kwa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni kielelezo cha hasira na chuki ya kimataifa dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita, na jinai dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.”

Ameongeza kuwa:“Huu pia ni mwito wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya utawala wa sheria na kumaliza ukwepaji wa adhabu kwa wanaotenda uhalifu wa kutisha dhidi ya watu wa Palestina."

Msemaji huyo ameendelea kulaani msimamo wa mataifa ya Ulaya kwa kusema:“Kwa kulegeza msimamo wake mbele ya utawala wa Israel, Ulaya siyo tu inavunjia heshima misingi ya sheria, bali pia inapuuza kabisa dhamira ya haki, na kuimarisha mazingira ya kutoadhibiwa—yenye athari mbaya kwa waathirika wasio na hatia na kwa ubinadamu wote kwa ujumla.”

Kauli hizi zimekuja muda mfupi baada ya kutangazwa kwa safari ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwenda Hungary. Serikali ya Budapest ilitangaza kuwa haitatekeleza agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu kumkamata Netanyahu, na hata ikatangaza kujiondoa katika chombo hicho cha kimataifa.

Ikumbukwe kuwa mwezi Novemba mwaka jana, Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, alimwalika Netanyahu kutembelea nchi hiyo, siku moja tu baada ya ICC kutoa hati ya kumkamata.

Hungary ni mojawapo ya wanachama waanzilishi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, na kisheria inalazimika kuwatia mbaroni wale wote waliotajwa katika hati za mahakama hiyo. Hata hivyo, Orbán alikataa wazi agizo hilo, akilieleza kuwa ni “lisilokubalika kabisa.”

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha